
UPINZANI wa watani wa jadi, Simba na Yanga umehamia mahakamani baada
ya Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji, kumpandisha kizimbani Mjumbe wa
Kamati ya Utendaji ya Simba, Musleh Al Rawah, akidaiwa kumpiga mwanaye.
Mjumbe huyo wa Simba alipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi, alisomewa shtaka
la kumjeruhi mtoto wa Manji, Mehboob Manji.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Genis Tesha, alidai
kuwa Al Rawah alifanya kosa hilo, Machi 8, mwaka huu katika Uwanja wa
Taifa uliopo Chang’ombe, baada ya kumalizika mchezo wa watani wa jadi
ulioisha kwa Simba kushinda bao 1-0 dhidi ya Yanga.
Tesha alidai kuwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa Al Rawah alimpiga
teke Mehboob katika sehemu mbalimbali za mwili ukiwamo uso na
kumsababishia majeraha mazito.
Al Rawah ambaye ni mfanyabiashara na raia wa hapa nchini anayetetewa
na Wakili Dk. Damas Ndumbaro, alikana shtaka hilo na upande wa mashtaka
ukadai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na hawapingi dhamana
kwa mshtakiwa.
Kwa upande wa Wakili Ndumbaro, naye aliomba mteja wake apewe dhamana.
Hakimu Moshi akitoa masharti ya dhamana kwa mshtakiwa huyo, alimtaka
awe na mdhamini mmoja ambaye anatoka katika taasisi inayotambulika ama
serikalini.
Baada ya mdhamini kujitokeza, upande wa mashtaka ulifanyia uhakiki
barua yake ndani ya saa moja kama ilivyoelekezwa na mahakama na
mshtakiwa akaachiwa huru.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 20, mwaka huu kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi umekamilika ama la.