KAMPENI: Chadema wasafiri kwa chopa kusaka majimbo Kanda ya Ziwa
Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Geita Alphonce
Mawazo akizungumza katika mkutano wa hadhara
uliofanyika juzi wilayani Sengerema. Kushoto ni
mtangaza nia wa chama hicho Hamis Tabasamu.
Picha na Michael Jamson
Mwanza. Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) Kanda ya Ziwa
Magharibi, kimeanzisha operesheni maalumu
kwa ajili ya kusaka ubunge katika majimbo
yote yaliyoko kwenye kanda hiyo ambayo
yanashikiliwa na Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Operesheni hiyo inayojulikana kama ‘tigitigi’,
ilianza juzi kwa kutumia usafiri wa helikopta
katika majimbo kadhaa, ikiwamo Jimbo la
Sengerema linaloshikiliwa na mbunge wa
sasa, William Ngeleja.
Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Geita
Alphonce Mawazo ni miongoni mwa makada
wa chama hicho waliofika katika jimbo la
Sengerema juzi, wakiambatana na kada wa
chama hicho anayetaka kutangaza nia ya
kuwania ubunge katika jimbo hilo, Hamis
Tabasamu.
Akihutubia kwenye mikutano ya hadhara
iliyofanyika katika vijiji tofauti kwa muda wa
dakika 30 katika kila kijiji, Mawazo alisema
wameanzisha operesheni hiyo kwa lengo la
kushinda ubunge kwenye majimbo yote
yaliyoko kwenye kanda hiyo ili kuleta
ukombozi wa kweli kwa wananchi.
“Wananchi naomba niwambie tumeanza na
Jimbo la Sengerema, tutapambana hadi hatua
ya mwisho ili kulikomboa jimbo hili. Tunataka
Kanda ya Ziwa iwe ya mfano, tutazunguka
kata zote na vijiji vyote katika mikoa ya Geita,
Simiyu, Mwanza, Tabora, Shinyanga na Mara
kuelimisha wananchi,” alisema Mawazo na
kuongeza’
“Pia naomba wananchi mjitokeze
kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la
Wapiga kura ili tuweze kupata nafasi ya
kufanya mabadiliko ya kweli mwezi Oktoba.
Ndugu zangu mapambano yameanza hakuna
kulala, huu ni wakati wetu Chadema,”
alisema.
Naye mtangaza nia wa jimbo hilo, Hamis
Tabasamu ambaye aliwahi kuwa diwani wa
Sengerema, alisema kuwa watafungua ofisi 78
za Chadema kwenye jimbo hilo ili wananchi
waweze kuwa na sehemu za kutoa
malalamiko yao kwa viongozi na
kuhudumiwa.
Alisema muda uliopo sasa ni wa kufanya
mabadiliko na kwamba kazi ya kutafuta
ukombozi Sengerema imeanza, hivyo ni
jukumu la wananchi wa eneo kuunga mkono
jitihada za chama hicho za kuwaletea
maendeleo endelevu.
“Mimi ni mtangaza nia wa jimbo hili nipo
tayari kushirikiana na nyie kuleta mabadiliko
ya kweli Sengerema. Tutafungua ofisi 78 hapa
na kazi zitafanyika kila kona ya jimbo hili ili
tuweze kuing’oa CCM hapa. Nia na sababu ya
kuing’oa CCM tunazo kwa kuwa ni ukweli
kwamba haijafanya kitu chochote katika
uongozi wake eneo hilo,”alisema Tabasamu.
0 comments:
Post a Comment