Hatutaahirisha Uchaguzi, yasema NEC
Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema haina mpango wa kutaka kuiongezea muda Serikali ya Awamu ya Nne kwa kuahirisha Uchaguzi Mkuu ambao kikatiba hutakiwa kufanyika Oktoba ya mwaka wa uchaguzi.
Kauli hiyo ya NEC imekuja baada ya viongozi wa vyama vya upinzani kuanza kuonyesha hofu kuwa Serikali inataka kuahirisha Uchaguzi Mkuu kwa kisingizio cha kutokamilika mapema kwa kazi ya uandikishaji wapigakura.
Uboreshaji wa Daftari la Wapigakura kwenye mji mdogo wa Makambako mkoani Njombe, ulianza Februari 23 kwa matarajio kuwa uandikishaji ungefanyika kwa wiki mbili, lakini haukuweza kukamilika kwa muda uliopangwa.
Jana mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema wanaoeneza taarifa hizo wanakusudia kuleta hofu kwa wananchi na kwamba tume hiyo haina malengo ya kuahirisha uchaguzi huo kama ilivyofanya kwenye Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkakati wa ushindi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema serikali inataka kujaribu kuahirisha Uchaguzi Mkuu kutokana na kusuasua kwa uboreshaji wa Daftari la Wapigakura unaofanywa kwa kutumia teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR).
Mbowe aliwahoji wanachama waliokuwapo ukumbini iwapo wapo tayari kwa Bunge kuongeza muda wa serikali ya awamu ya nne, ambapo wote walisema “hapana”.
Jaji Lubuva alisema kuwa suala la Uchaguzi Mkuu ni la Kikatiba chini ya Ibara ya 65 ya Katiba ambayo inasema kwamba maisha ya Bunge ni miaka mitano na ndio muda wa Rais aliye madarakani.
“Tume asilani haina utaratibu wowote wa kuwezesha serikali ibaki madarakani zaidi ya kipindi ambacho kimepangwa na Katiba, na isitoshe Rais wetu ni mtu ambaye anafuata Katiba, na msikivu, hivyo sidhani kama anaweza kutumia mbinu zozote kwa kutumia tume ya uchaguzi akabaki madarakani,” alisema Jaji Lubuva na kuongeza kuwa hata rais mwenyewe amesema anasubiri siku ifike aondoke madarakani.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa wanasiasa wanaozungumzia kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu na mipango ya kumwongezea Rais Kikwete muda wa kukaa madarakani wanawatia hofu wananchi ili wasiende kujiandikisha.
“Wanasiasa ni bora wakaeleza sera zao kuliko kuwa wataalamu wa BVR,” alisema.
Kuhusu kuahirishwa kwa Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa, mwenyekiti huyo alisema uamuzi huo ulifikiwa kutokana na kuwapo kwa vifaa vichache, lakini hivi sasa vifaa hivyo vinatarajiwa kuwepo vya kutosha.
Jaji Lubuva alisema uandikishaji mkoani Njombe unamalizika leo na awamu ya pili itakayoanza Aprili 24 mwaka huu itaihusisha mikoa ya Iringa, Lindi, Ruvuma na Mtwara.Alisema wanatarajiwa mashine 1,600 za BVR zitawasili wakati wowote kwa ajili ya kazi hiyo. Aliongeza kuwa mashine nyingine 1,600 zinatarajiwa kuwasili nchini kwa ajili ya mikoa ya Dodoma, Mbeya, Katavi na Rukwa na uandikishaji kwenye mikoa hiyo utaanza Mei 2, 2015.
Mashine 1,152 zinatarajiwa kuwasili nchini kwa ajili ya mikoa ya Singida, Tabora, Kigoma na Kagera. Tarehe ya uandikishaji katika mikoa hiyo bado haijapangwa.
Hata hivyo, mara kadhaa Jaji Lubuva alikuwa akinukuliwa akisema kuwa Kura ya Maoni ya Katiba inayopendekezwa ingefanyika Aprili 30 kama ilivyokuwa imepangwa licha ya wadau mbalimbali kuonyesha hofu kutokana na mwenendo wa uandikishaji wapigakura.
Jaji Lubuva pia alivitaka vyama vya siasa kuacha kuingilia maamuzi ya tume yake kwa kile alichoeleza kuwa kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa.
Akizungumza kwa kujiamini, Jaji Lubuva alisema baadhi ya wanasiasa wanakosea kwa kufananisha namna mashine za BVR zilivyoshindwa kufanya kazi Kenya na Nigeria.
Alisema Kenya ilitumia siku 36 kuandikisha watu milioni 14 na Nigeria ilitumia siku 21 kuandikisha watu milioni 70, na akasisitiza kuwa Tanzania itaandikisha wapigakura wote kabla ya Julai mwaka huu.
Mkurugenzi Manunuzi na Logistiki wa NEC, Gregory Kaijage alisema BVR zimetengenezwa na kampuni ya Lithotech Export ya Afrika Kusini baada ya kushinda tenda.
“Lakini ili yasitokee maswali mengine ambayo tunayategemea, Lithotech ina uwezo wa kuwasainisha mkataba watu wengine, tumebaini wapo watu wa China…na vifaa vingine vinatoka nchi nyingine,” alisema Kaijage.
Naibu Katibu na Mkuu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa NEC, Dk Sisti Cariah alisema kama tume hiyo ingekuwa na mashine zote hivi sasa wangeandikisha kwa siku 28 tu nchini nzima.
“Kwa mujibu wa rekodi za sensa tungekuwa na uwezo tungeandikisha watu wote milioni 23.9 wanaotarajiwa kupiga kura,” alisema Cariah.
0 comments:
Post a Comment