Watawala na wasomi watakiwa kuwa wabunifu ili kuleta maendeleo nchini.
Watawala, watendaji wa serikali pamoja na wasomi nchini wametakiwa kutoa fikra za kibunifu kwa kutumia sayansi na teknolojia juu ya namna ya kuliwezesha taifa kupiga hatua za maendeleo ya kiuchumi kwa kutumia rasilimali zilizopo pamoja na kuenzifikra za hayati Nyerere za kujenga umoja wa kitaifa na kuziba nyufa za matabaka ambayo yameanza kujidhihirisha miongoni mwa watanzania.
Changamoto hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na waziri mkuu
mstaafu Mh David Cleopa Msuya katika uzinduzi wa kavazi la Mwalimu
Nyerere na kuongeza kuwa tawala mbalimbali zilizopita hapa nchini kwa
namna moja ama nyingine imeshindwa kutatua changamoto ya kulifanya taifa
kupiga hatua za maendeleo kiuchumi kwa kutumia rasilimali zilizopo bila
ya kutegemea wahisani na kwamba ni jukumu la watawala wa sasa pamoja na
wasomi kutoa majibu kwa kutumia fursa ya maendeleo ya sayansi na
teknolojia iliyopo.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa tume ya sayansi na teknolojia Dk
Hassan Mshinda amesema rasilimali pekee bila ya ubunifu wa kutosha
hazitoshi kulisaidia taifa kupiga maendeleo ya kiuchumi huku mkurugenzi
wa kavazi Prof Issa Shivji akiwataka viongozi wa serikali kuwa na hulka
ya upole na unyenyekevu jambo linalotoweka miongoni mwa viongozi wa
sasa.
Baadhi ya viongozi wa kisiasa na wasomi waliohudhuria uzinduzi huo
wamesema ni vyema taifa kutochukulia kwa mzaha amani na utulivu wa nchi
uliopo hivi sasa na badala yake waziba nyufa zilizoanza kujitokeza
sambamba na viongozi kutenda vile wanenavyo.
0 comments:
Post a Comment