Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja awatumia Zitto, Mengi, Manji kujitetea
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja jana alimtaja Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe na baadhi ya
matajiri wanaowafadhili wabunge nchini, kama sehemu ya utetezi wake
mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma.
Ngeleja ambaye amewahi kuwa Waziri wa Nishati na
Madini alikuwa anajitetea mbele ya baraza hilo kuhusiana mgawo wa Sh40.4
milioni, aliopata kutoka kwa mfanyabiashara na mmiliki wa Kampuni ya
VIP Engeneering & Marketing Limited, James Rugemalira.
Pamoja na kudai kuwa mgawo huo haukuwa na mgongano
wa masilahi, Ngeleja aliibua tuhuma mpya akihoji ni kwa nini Zitto
hakuhojiwa na baraza kwa kutuhumiwa kupokea fedha kutoka katika Kampuni
ya Pan African Power Solution (PAP), ambayo pia inahusishwa katika
kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa ndani ya Benki Kuu ( BoT)
wala tuhuma za kufadhiliwa na Mfuko la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Mashtaka dhidi ya Ngeleja
Akimsomea mashtaka, Mwanasheria wa Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma, Mwanaarabu Talle alidai kuwa Ngeleja akiwa
kiongozi wa umma alipokea fedha hizo kwenye akaunti yake namba
0011010265260 katika Benki ya Mkombozi na hivyo kusababisha mgongano wa
kimaslahi.
Wakili Talle alidai kuwa kwa kupokea fedha hizo
kutoka kwa kampuni hiyo, Ngeleja alikiuka kifungu cha 6(e) cha Sheria ya
Maadili ya Viongozi wa Umma, kinachozuia kiongozi wa umma kujiingiza
katika mgongano wa masilahi.
Pia wakili Talle alidai kuwa Ngeleja alijipatia manufaa ya kifedha kinyume cha kifungu cha 12 (1) (e) cha sheria hiyo.
Ushahidi wa sekretarieti
Baada ya kumsomea mashtaka hayo, Ngeleja alikana
na shahidi wa Sekretarieti, Waziri Yahya akiongozwa na Wakili Talle
alidai kuwa baada ya kuchunguza walibaini kuwa Ngeleja alipewa
Sh40,425,000 kutoka VIP Engeneering & Marketing Februari 12, 2014.
Alidai kitendo cha Ngeleja cha kupokea pesa hizo
kumekiuka sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo hairuhusu kuomba,
kupata au kupokea fedha.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, walibaini kuwa mwaka
2007 Ngeleja alikuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na kwamba kuanzia
2008 hadi 2012 alikuwa Waziri wa Nishati na Madini ambapo aliendelea na
majukumu ya kusimamia utekelezaji wa mkataba kati ya Tanesco na IPTL
ambayo VIP ilikuwa na hisa.
0 comments:
Post a Comment