Katiba ‘mwiba’ kwa wapinzani
SIKU moja
baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam,
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kuonya juu ya waraka wa maaskofu wa
kutaka wananchi waikatae Katiba Inayopendekezwa, wanaoisakama Katiba
hiyo wamezidi kubanwa na kuonekana wasioitakia mema Tanzania.
Pamoja na
kuunga mkono `karipio’ la Kardinali Pengo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM
-Zanzibar, Vuai Ali Vuai amesema viongozi wa kambi ya upinzani na
washirika wao hawaitaki Katiba Inayopendekezwa kwa sababu wanajua wazi
kwamba ndiyo mwarobaini wa ufumbuzi wa kero zote, zikiwemo za Muungano
zilizokuwa zikipigiwa kelele na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar (SMZ) wakiwemo wa upinzani.
Vuai
alisema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya wajumbe wa
Sekretarieti ya mikoa na wilaya ya CCM kwa ajili ya kupigwa msasa na
kujitayarisha kutoa mafunzo ya Katiba Inayopendekezwa kwa wanachama
katika shehia mbalimbali, Kendwa, mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema
wapinzani wanajua fika kuw
a Katiba Inayopendekezwa imezipatia ufumbuzi
kero zote za Muungano zilizokuwepo awali kwa hivyo hawana jipya na hilo
ni pigo kwao kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu.
“Wananchi
wengi wanawashangaa wapinzani na viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF)
kwa sababu wao walipokuwa Baraza la Wawakilishi walikuwa wakilalamika
kero za Muungano na kukubaliana kuzipatia ufumbuzi katika Bunge Maalumu
la Katiba ambalo mara baada ya kuanza kikao chake walisusia…” alisema.
Alitaja
suala la nishati na mafuta ambalo awali lilikuwa katika orodha ya mambo
ya Muungano, lakini wajumbe wa Bunge la Katiba walikubaliana na kuipa
uwezo Zanzibar sasa kushughulikia rasilimali hiyo wenyewe.
Alisema
tayari wawekezaji mbalimbali wameonesha nia ya kuja nchini kuwekeza
katika sekta ya nishati pamoja na nchi nyingine kukubali kuwasomesha
vijana wa Kitanzania katika sekta hiyo, lakini wapinzani wamekuwa
wakiwavunja moyo wananchi kwa kuwashawishi kuikataa Katiba
Inayopendekezwa ambayo maslahi yake kwa Zanzibar na Watanzania kwa
ujumla ni makubwa.
Vuai
alifafanua na kusema viongozi wa CUF wameonesha udhaifu mkubwa na kasoro
katika uongozi wa nchi huku wakiweka mbele maslahi yao binafsi kuliko
faida ambayo wananchi wa Zanzibar watapata.
Aliwataka
viongozi watakaokwenda kwa wananchi kuichambua Katiba Inayopendekezwa
kifungu kwa kifungu zaidi katika vifungu ambavyo vimelenga na kutaja
maslahi ya Zanzibar katika mambo ya Muungano.
Alisema
CUF katika Katiba Inayopendekezwa walikuwa wakitaka suala moja tu la
Muungano wa mkataba na baada ya kukataliwa rai yao hiyo walikuja na
Muungano wa Serikali tatu, huku wakikubali kuunganisha nguvu na baadhi
ya vyama vya upinzani vilivyozaa umoja unaojulikana kama Ukawa.
Usomaji wa Katiba
Wakati
Vuai akifichua kile kinachoonekana kuwa ni siri ya wapinzani na
washirika wake kuikataa Katiba Inayopendekezwa, Serikali imesisitiza
kuwa, wananchi wanapaswa kuachiwa fursa ya kujiamulia wenyewe juu ya
aina ya Katiba wanayoitaka, maamuzi wanayoweza kuyafanya baada ya kusoma
kwa kina Katiba Inayopendekezwa.
Akizungumza
jana jijini Dar es Salaam wakati akikabidhi nakala ya Katiba
Inayopendekezwa kwa taasisi na makundi mbalimbali, Waziri wa Katiba na
Sheria, Dk Asha-Rose Migiro alisema: “Wananchi wanapaswa wapewe fursa
waisome Katiba Inayopendekezwa kisha wachukue maamuzi wao wenyewe bila
kushinikizwa na mtu, au kikundi chochote kuhusiana na kupiga kura.”
Akiuzungumzia
waraka wa Baraza la Maaskofu (TEC) na Jukwaa la Wakristo uliotolewa na
kusomwa sehemu mbalimbali ikiwa pamoja na nyumba za ibada, Dk Migiro
alisema amefurahishwa na kauli ya Kardinali Pengo ya kuwaonya viongozi
wa dini kutoingilia uhuru wa waumini wao, kwani kwa kufanya hivyo ni
kwenda kinyume na maadili ya kazi yao.
“Nimefurahishwa
sana na kauli ya Kardinali Pengo na kila mtu anapaswa aheshimu kauli
hiyo. Pindi muda ukifika wa kupiga kura hapo Aprili 30 mwaka huu, apige
kura kwa kujiamulia mwenyewe,” alisema Dk Migiro aliyesisitiza hakuna
mabadiliko ya tarehe juu ya siku ya kupiga Kura za Maoni.
Akimkaribisha
Dk Migiro kukabidhi nakala za Katiba Inayopendekezwa, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Katiba na Sheria, Maimuna Tarishi alisema jumla ya nakala
658,700 kati ya zaidi ya milioni 2 zinatarajiwa kugawiwa kwa taasisi za
kidini, wizara za serikali na mashirika ya umma na yasiyo ya kiserikali.
TEC, CCT wakosolewa
Mmoja wa
wasomi na mchambuzi mahiri wa masuala ya siasa nchini, Dk Benson Bana wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amezungumzia tamko la TEC na CCT
na kusema halina hekima na limelenga kuligawa taifa.
“Nilipousoma
sikuamini kama kweli umetolewa na maaskofu mpaka pale nilipoona saini
zao. Inasikitisha kuona maaskofu ambao wana nafasi kubwa katika jamii na
ni kimbilio pale panapokuwa na shida kutoa tamko la kuegemea upande
mmoja,” alisema.
Alisema
si vyema kwa maaskofu kutoa tamko kama hilo katika mazingira ya sasa na
kuwa walitakiwa kutafakari kabla ya kutoa waraka huo.
“Labda
watuambie kuwa TEC na CCT ni vikundi vya kiraia kwa kuwa na upande, na
tamko kama hili linafanya tuhoji taifa linakwenda wapi hasa katika
madaraka, yaliyotokea Rwanda na Somalia yalianza watu wenye madaraka
ambao wana ushawishi mkubwa katika koo zao na dini zao kuonesha misimamo
yao.”
Alisema
maaskofu wanatakiwa kujua kuwa mradi wa kujenga taifa kuwa taifa la
amani ni endelevu na ulianza mwaka 1961 nchi ilipopata uhuru na bado
kuna wajibu kuendelea kujenga amani ya nchi.
“Kama leo
wametoa tamko hilo Wakristo na Waislamu nao watoe yao na jumuia
nyingine zitoe zao unadhani athari yake itakuwaje?,” alisema na kuhoji
maaskofu walikuwa wapi kukosoa Katiba ya 1977 ambayo ina mapungufu. Bana
aliongeza: “Suala la wananchi kupigia kura ya maoni ya Katiba
Inayopendekezwa ni haki ya Watanzania, na sasa maaskofu wasinyang’anye
haki hiyo, ya Kaisari wamwachie Kaisari.”CHANZO:HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment