Cheka atolewa jela, apewa kifungo cha nje
BONDIA nguli nchini, Francis Cheka, jana alitolewa rumande na kupewa
kifungo cha nje, huku akitakiwa kuripoti katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya
ya Morogoro Mjini kila siku kwa ajili ya shughuli za kijamii.
Hatua hiyo ya Cheka kutolewa rumande imekuja baada ya kukata rufaa
akiiomba mahakama impe kifungo cha nje kutokana na majukumu ya kifamilia
aliyokuwa nayo, huku akidai anatategemewa kwa kila kitu na familia
yake.
Hata hivyo, Cheka ametakiwa kutofanya kosa lolote ndani ya miaka
mitatu ya kifungo chake, kwani akipatikana na hatia nyingine atarudishwa
jela na kutumikia kifungo alichonacho mara mbili.
Mara baada ya kupata hukumu ya mwanzo, bondia huyo akizungumza na
MTANZANIA alisema kifungo alichopewa kina mkono wa watu wenye lengo la
kutaka kuchafua jina lake na maisha yake.
“Nimeshangazwa kusomewa kuwa nimekiri kosa la kumpiga mlalamikaji
wakati katika maelezo yangu nilikana shtaka, hivyo ni wazi kesi hii
ilipangwa kuvurugwa ili niweze kufungwa na kupotezwa katika ulimwengu wa
wanamasumbwi,” alisema.
Hata hivyo, bondia huyo baada ya kutoka alikutana na familia yake, jamaa na marafiki ambao walijitokeza kumlaki.
0 comments:
Post a Comment